Jioni ya leo mikiki mikiki ya kombe la FA inaendelea ambapo mchezo wa kukata na shoka kati ya Wajelajela Tanzania Prisons dhidi ya Yanga utapigwa uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga
Huu ni mchezo mwingine wa kibabe utakaozikutanisha timu hizo kwa mara ya tatu msimu huu
Michezo yote miwili ya kwenye ligi ilimalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1
Leo lazima mshindi apatikane ambaye atatinga robo fainali ya michuano hiyo ambayo bingwa wake atajihakikishia tiketi ya kushiriki michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Akiungana na timu itakayomaliza katika nafasi ya tatu kwenye ligi
Kwa Yanga huu ni mchezo ambao ushindi ni matokeo yanayohitajika zaidi hasa baada ya kupoteza mchezo uliopita kwenye ligi kuu kwa kufungwa bao 1-0 na Azam Fc
Yanga iliweka kambi mkoani Mbeya tangu Jumanne, jana wakaingia Sumbawanga na jioni wakafanya mazoezi yao ya mwisho katika uwanja wa Nelson Mandela
Kocha Nasreddine Nabi atawakosa baadhi ya wachezaji muhimu ambao wanatumikia adhabu ya kadi tatu za njano
Feisal Salum, Mukoko Tonombe na Michael Sarpong hawatakuwa sehemu ya mchezo huo
Hata hivyo Yanga ilisafiri na kikosi chake kamili na bila shaka nafasi zao zitachukuliwa na wachezaji wengine
Mchezo utaunguruma kuanzia saa kumi kamili Alasiri