Kocha Mkuu wa Yanga Mohammed Nasreddine Nabi pamoja na wachezaji wake leo wamebeba matumaini ya mamilioni ya Wanayanga wanaosubiri mchezo wa kukata na shoka dhidi ya Simba ambao utapigwa baadae leo katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Ni mechi kubwa inayotarajiwa kuwa na ushindani mkali, hesabu za Nabi kwa kiasi kikubwa zinaweza kuamua matokeo ya mchezo huo
Jambo jema kwake ni kuwa Kocha wa Simba Didier Gomes hawezi kumtabiri ataingiaje katika mchezo huo kwani hana zaidi ya wiki tatu tangu alipojiunga na Yanga
Baada ya kupoteza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Azam Fc, maboresho katika kikosi chake yalionekana kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons ambao Yanga walishinda bao 1-0
Wananchi waliishuhudia timu yao ikicheza kandanda safi katika mchezo huo na kwa kiasi kikubwa alirejesha imani ya mashabiki kuelekea mchezo wa leo
Nabi atawakabili Simba akiwa na kikosi chake kamili japo kuna hatihati ya baadhi ya wachezaji kukosekana kutokana na kuwa majeruhi
Kiungo Carlos Carlinhos na beki wa kushoto Yassin Mustafa wanatajwa kuwa watakosa mchezo huo
Yassin alipata majeraha kabla ya ujio wa Nabi. Carlinhos alicheza mechi zote mbili chini ya Nabi
Lakini eneo analocheza Carlinhos lina wachezaji mbadala kama Haruna Niyonzima na Feisal Salum wanaoweza kutumika
Utabiri wa kikosi kinaweza kuwa hivi;
Langoni huenda akasimama Metacha Mnata ambaye alikuwa na mchezo mzuri sana kule Sumbawanga dhidi ya Tanzania Prisons ambapo Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0
Walinzi wa pembeni nao wanaweza kubaki walewale waliotumika Sumbawanga, Kibwana Shomari na Adeyum Saleh
Hata eneo la safu ya ulinzi wa kati linaweza lisiwe na mabadiliko, nahodha Lamine Moro na Abdallah Shaibu Ninja wanaweza kusimama
Mukoko Tonombe ataendelea kubaki katika eneo lake la kiungo mkabaji huku upande wa wingi ya kulia pengine Tuisila Kisinda 'TK Master' atarejea
Wingi ya kushoto Ditram Nchimbi 'Duma' huenda akaanza wakati Feisal Salum/Haruna Niyonzima mmoja anaweza kuchukua mikoba ya Carlinhos eneo la kiungo cha uchezeshaji
Yacouba Songne ndiye mshambuliaji wa Yanga ambaye yuko katika kiwango bora cha kupachika mabao, hapaswi kukosekana leo
Pengine ataongoza safu ya ushambuliaji sambamba na Saido Ntibazonkiza 'Antibiotic' ambaye katika kikosi cha Nabi amekuwa akitumika kama namba 10
Nabi ni muumini wa soka la kushambulia, akipendelea timu yake imiliki mpira pia, pengine mfumo atakaoingia nao leo ni 4-1-4-1
Katika Mkutano na Wanahabari jana, Nabi aliwaahidi mashabiki wa Yanga kuwa watarajie burudani nzuri kutoka kwa timu yao
Aidha akaongeza kuwa mchezo huo utakuwa kielelezo cha kuimarika kwa soka la Tanzania