Kikosi cha Yanga jioni ya leo kitashuka katika uwanja wa Majaliwa, Ruangwa kuikabili Namungo Fc ukiwa ni mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Baada ya sintofahamu iliyojitokeza na kupelekea mchezo dhidi ya watani Simba kupigwa kalenda, Yanga ilihamishia hesabu zake mchezo dhidi ya Namungo Fc ambao pia una umuhimu wa kipekee
Ni mchezo wa nne kuzikutanisha timu hizo kwenye ligi tangu Namungo Fc walipopanda daraja msimu uliopita
Michezo yote mitatu iliyopita ilimalizika kwa matokeo ya sare hivyo Wananchi watakuwa wakisaka ushindi wao wa kwanza dhidi ya Namungo Fc
Yanga iliweka kambi ya kujiandaa na mchezo huo mkoani Mtwara na jana wakatua Ruangwa na jioni wakafanya mazoezi yao ya mwisho katika uwanja wa Majaliwa
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amepata wasaa wa kuisoma Namungo Fc, akifuatilia matokeo ya mechi za nyuma na bila shaka leo atakuja na mbinu ambazo zitaihakikishia ushindi Yanga
Wananchi wanazihitaji alama zote tatu, ni kauli iliyotolewa na Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli
Bumbuli amesema bado wako kwenye mbio za kuwania ubingwa, hivyo siku ya leo hawapaswi kupoteza mchezo
Kikosi cha Yanga leo kinatarajiwa kukosa huduma ya baadhi ya wachezaji wake muhimu ambao ni majeruhi
Carlinhos, Abdallah Shaibu 'Ninja', Yassin Mustafa na Mapinduzi Balama wote wamebaki jijini Dar es salaam wakiendelea kuuguza majeraha
Je Wananchi watapata ushindi wao wa kwanza dhidi ya Namungo Fc katika ligi leo? Majibu yatapatikana baada ya dakika 90 za mchezo utakaopigwa kuanzia saa kumi Alasiri