Yanga imetakata uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma leo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa ligi kuu
Wananchi walipania kuondoka na alama zote tatu tangu mapema tu na walifanikiwa kufunga mabao yao yote mawili katika kipindi cha kwanza
Krosi murua ya Kibwana Shomari ilitua kichwani kwa Yacouba Songne aliyeiandika Yanga bao la kuongoza kwenye dakika ya 27
Wakati JKT Tanzania wakijiuliza nini kimetokea, Tuisila Kisinda 'TK Master' akaipatia Yanga bao la pili kwenye dakika ya 30 baada ya kumalizia krosi ya Ditram Nchimbi iliyowapita walinzi wa JKT Tanzania kabla ya kumfikia



Yanga ilishambulia kwa nguvu katika kipindi chote cha kwanza na kwa kiasi kikubwa mbinu za kocha Nasreddine Nabi zilifanikiwa
Katika kipindi cha pili JKT Tanzania walijaribu kucheza mpira kusaka angalau bao la kufutia machozi lakini safu ya ulinzi ya Yanga iliyokuwa chini ya mabeki visiki Dickson Job na Bakari Nondo, wakisaidiwa na walinzi wa pembeni Kibwana Shomari na Adeyum Salem mbele ya mlinda lango Metacha Mnata, hakukuwa na njia ya kupita
Ni ushindi ambao Yanga waliuhitaji sana kuhakikisha wanaendelea kusalia katika nafasi ya pili sasa wakiwa na alama 61 kama walivyo watani zao Simba ambao wanaongoza ligi kwa tofauti ya mabao
Baada ya mchezo huo Yanga Wananchi wanaelekeza nguvu zao kwenye mchezo wa robo fainali kombe la FA dhidi ya Mwadui Fc ambao utapigwa May 25 mkoani Shinyanga