Kesho Jumanne kikosi cha Yanga kitashuka uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga kuikabili Mwadui Fc katika mchezo wa robo fainali kombe la Shirikisho la Azam (ASFC)
Yanga itakuwa ikisaka nafasi ya kutinga nusu fainali kuifuata Biashara United ambayo ilitangulia jana kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo Fc
Pamoja na kuwa Mwadui Fc tayari wameteremka daraja, Yanga haitauchukulia mchezo huu kirahisi
Mkufunzi wa Yanga Nasreddine Nabi amesema ni mchezo muhimu kwake na kikosi chake kwani utatoa nafasi ya kuingia hatua ya nusu fainali na kulikaribia taji la Shirikisho la Azam ambalo linatoa nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.
"Naamini utakuwa mchezo mgumu na wenye upinzani, kwani kila timu itakuwa ikiwania nafasi ya kuingia nusu fainali japokuwa wenyeji Mwadui watakuwa nyumbani mbele ya mashabiki wao, hivyo tunapaswa kuwa makini sana ili tuweze kutimiza malengo yetu"
"Tunapaswa kuongeza umakini hasa sehemu ya ulinzi tusiruhusu bao na nafasi ya ushambuliaji watumie kila nafasi tutakazo pata ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali," alisema Nabi
Hii ni mara ya pili msimu huu Yanga inachuana na Mwadui Fc uwanja wa CCM Kambarage, mara ya kwanza walikutana kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza ligi kuu ya Vodacom Yanga ikifanikiwa kuondoka na ushindi wa mabao 5-0