Siku za karibuni baadhi ya wachezaji wa Yanga wameondolewa kambini kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu
Alianza nahodha Lamine Moro na siku moja kabla ya mchezo dhidi ya Mwadui Fc, wachezaji wengini Metacha Mnata na Michael Sarpong wakaondolewa kambini kwa makosa ya utovu wa nidhamu
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli ametoa ufafanuzi wa sintofahamu hiyo ambapo amesema inatokana na msimamo wa Kocha Mkuu Nasreddine Nabi
Bumbuli amesema Nabi ameweka msimamo kwa wachezaji wote kuhakikisha wanafuata maelekezo na kufuata taratibu
"Zamani kulikuwa na tabia ambayo ilianza kuzoeleka na kuonekana kama ni jambo la kawaida. Mchezaji anaweza akachelewa kufika mazoezini au asifike kabisa bila ya kutoa taarifa yoyote. Wengine walikuwa wakizima hata simu zao halafu siku wakija mazoezini ndio wanasema sababu iliyowafanya wasionekane siku ya nyuma"
"Mwalimu wa sasa (Nabi) hataki mambo hayo. Mchezaji ukiwa na tatizo unapaswa kutaarifu viongozi, kama ni majeruhi au unaumwa lazima madaktari wa timu wawe na taarifa zako"
"Hii tabia ya kufanya mambo kienyeji ndio inawaingiza matatizoni baadhi ya wachezaji kwani benchi la ufundi sasa limeweka mkazo, hakuna mazoea tena," alisema Bumbuli
Siku aliyosaini mkataba wa kuinoa Yanga, Nabi alisisitiza kuwa hatakuwa tayari kufanya kazi na wachezaji ambao hawana nidhamu
Nabi anaishi katika ahadi aliyoitoa kwa Wanayanga katika jitihada za kuisuka upya Yanga