Baada ya kuvuka hatua ya nusu fainali ya kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) uongozi wa Yanga umesema watapambana kuhakikisha wanatwaa taji hilo msimu huu
Ushindi wa mabao 2-0 juzi dhidi ya Mwadui Fc, uliihakikishia Yanga kutinga nusu fainali sasa ikitarajiwa kucheza na Biashara United katika mchezo ambao utapigwa uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora Juni 14-15
Huu ni msimu wa tatu mfululizo Yanga inafanikiwa kutinga nusu fainali. Hata hivyo haijaweza kuvuka hatua hiyo katika misimu miwili iliyopita
Kocha wa makipa Razack Siwa amesema wamelenga kushinda taji hilo ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya CAF msimu ujao
Aidha kocha huyo raia wa Kenya amesema kikosi kinaendelea kuimarika, akiridhishwa na kiwango kinachoonyeshwa na wachezaji
"Tulipokea kwa furaha matokeo ya ushindi dhidi ya Mwadui Fc, wachezaji walicheza vizuri na wemetuwezesha kuffikia malengo ya kushinda mchezo huo"
"Tumeweka malengo ya kufanya vizuri kwenye michuano hii, tutapambana hadi dakika ya mwisho bila kuangalia timu nyingine inafanya nini. Sisi tunaendelea na mapambano na mwisho wa michezo ndipo kila kitu kitaamua," alisema Siwa
Yanga, Simba, Azam Fc na Biashara United ndio timu zilizofanikiwa kuingia nusu fainali
Wakati Yanga ikisubiri kucheza na Biashara United, watani zao Simba watawakabili Azam Fc katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Majimaji, Songea
Mchezo wa fainali utapigwa uwanja wa Lake Tanganyika, mkoani Kigoma