Tangu jana wamejitokeza wachambuzi na wanahabari ambao wanampigia 'debe' kiungo mshambuliaji wa klabu ya Simba Ibrahim Ajibu arejeshwe Yanga
Licha ya Yanga kusisitiza kuwa hawawezi kumsajili Ajibu kwa kuzingatia mazingira ya sasa, bado mjadala umeendelea kuvuma kwenye mitandao ya kijamii
Mwisho wa siku maamuzi ya mwisho wanayo Yanga wenyewe, hao wanaopiga kelele hawawezi kumsaidia
Tatizo lilianzia hapa
Wakati mwingine mchezaji unapaswa kuwa makini pale unapoondoka timu moja kwenda timu nyingine kwani unaweza kufanya makosa ambayo yatakugharimu baadae
Ajibu alikuwa mmoja wa wachezaji waliokubalika sana Yanga. Alifanua mambo makubwa katika muda mfupi aliokuwa na Wananchi
Wakati timu ikipita kwenye kipindi kigumu mwaka 2018, aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera alikuja na pendekezo la kuwataka mashabiki waichangie timu yao
Ilifunguliwa akaunti maalum kwa ajili ya kupokea fedha hizo. Ajibu akiwa nahodha, alikuwa mmoja wa waweka saini benki kwa fedha yoyote iliyotolewa kwenye akaunti hiyo
Wakati huo Wananchi walikuwa na imani kubwa sana na Ajibu. Ni kwa sababu aliibeba Yanga, mguu wake ulikuwa sababu ya furaha ya Wananchi. Alifunga na kutengeneza pasi nyingi za mabao yaliyokuwa yakiwekwa kambani na Heritier Makambo
Ndio maana pale mkataba wake ulipomalizika, mashabiki waliutaka uongozi kutumia gharama yoyote kuhakikisha Ajibu haondoki
Aliwekewa fungu la kutosha, kuna viongozi walikwenda kuzungumza mpaka na mama yake wakimuomba amshawishi Ajibu asaini mkataba mpya Yanga
Ajibu alitoa kauli moja tu, kuwa fedha haziwezi kuzidi mapenzi, akimaanisha kuwa yeye ameamua kurejea Simba kwa sababu ni klabu anayoipenda
Sasa leo mapenzi na Simba yameisha? Ana sababu gani tofauti itakayowashawishi viongozi wa Yanga wamsajili?
Kama ni ubora hakuna anayefahamu, ni muda hajaonekana uwanjani. Ligi kuu inaelekea ukingoni lakini sidhani kama amecheza zaidi ya mechi tano
Mchezaji hapigiwi debe asajiliwe, uwezo wake utambeba. Pia anapaswa kuwa na mahusiano mazuri na timu anayokwenda kujiunga nayo
Hakuna mchezaji anaweza kufanikiwa katika timu kama mashabiki hawamtaki