Jemedari Said ni Meneja wa mlinda lango Metacha Mnata ambaye uongozi wa Yanga umemsimamisha kufuatia kitendo cha kuwatukana mashabiki baada ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ruvu Shooting uliopigwa jana uwanja wa Benjamin Mkapa
Jamedari amekiri kuwa mteja wake alifanya makosa kwa kuwatukana mashabiki ambao kimsingi ndio mabosi tena ikiwa alifanya makosa uwanjani kwa kuruhusu bao jepesi
Jemedari amesema Metacha amekiri kuwa bao la pili walilofunga Ruvu Shooting lilitokana na makosa yake, alidhani mpira ulikuwa ukitoka nje
"Nilizungumza nae, amekiri alifanya makosa, amesema goli alilofungwa ilikuwa ni timing mbovu, alijua mpira utatoka nje"
"Tulifanya kikao baada ya mchezo, nikamwambia kwa Yanga Sc ninayoijua mimi, haitafika kesho lazima uadhibiwe na kweli ikatokea akaadhibiwa. Pia nimemwambia asubiri adhabu nyingine kutoka TFF kwani watatumia ushahidi wa video aliyoonyesha mashabiki ishara ya tusi"
"Metacha alifanya kosa kiwanjani lakini kibaya zaidi akafanya kosa kubwa zaidi kuwatusi Mabosi wake (Mashabiki), hatua waliyochukua viongozi wa Yanga kumsimamisha wako sahihi kwa sababu alifanya mambo ya hovyo," alisema Jemedari
Aidha katika hatua nyingine, Jemedari amekanusha tetesi zinazomuhusisha Metacha na klabu ya Simba akisisitiza kuwa hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika kwani wanaheshimu mkataba wake na Yanga
"Hatujaongea na klabu yoyote, Metacha ni mali ya Yanga nashangaa hizo taarifa zimetoka wapi. Mkataba wake na Yanga unaelekea ukingoni, sisi tuko tayari kusaini mkataba mpya lakini Yanga wenyewe ndio wanaochelewesha pengine kwa sababu kuna deni la nyuma. Lakini hilo halituzuii kuongeza mkataba mwingine"
"Nafahamu, mchezaji akibakiza miezi (6) ni ruksa kuongea na timu nyingine lakini lazima utoe taarifa kwa timu yake, kinyume chake ni kutenda kosa"