Mzee Mpili anaendelea kutamba kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari akiwapa 'mhaho' watani Simba
Akihojiwa na Wasafi Fm mapema leo, Mpili amesema baada ya kipigo cha bao 1-0 walichowapa Simba juzi, wanajua timu hiyo imeanza 'harakati' kuelekea mchezo wa fainali kombe la FA utakaopigwa mkoani Kigoma
Mpili amewapa pole akidai tayari wamechelewa kwani nayo wanapigwa
"Tunajua Simba inajipanga kulipa kisasi kwenye mchezo wa Fainali ya FA lakini tayari wamechelewa Kigoma wanakufa tena na shughuli imeisha, tunawapiga tena," alisema Mpili
Aidha, Mzee Mpili ambaye amejizolea umaarufu siku za karibuni, amesema Yanga haijawahi kupoteza mchezo wowote dhidi ya Simba kombe likiwa uwanjani
"Labda kama mmeifahamu Yanga leo, sisi miaka yote hatufungwi na Simba kombe linapokuwa uwanjani. Nawaambia tu hizi mechi mbili zinazokuja waangalie sana wakizubaa tunapiga zote," alitamba Mzee Mpili
Katika hatua nyingine, Mzee Mpili amemtahadharisha msemaji wa Simba Haji Manara kuwa anapaswa kutimiza ahadi yake ya kumpa kitita cha Tsh Milioni Moja baada ya ushindi wa Yanga
Manara alitoa ahadi hiyo kabla ya mchezo uliopigwa Jumamosi ambapo alisema kama Yanga itaifunga Simba basi yeye atatoa fedha hizo kumpatia Mzee Mpili
Baadhi ya mashabiki wa Simba wamejitolea kuchangishana fedha hizo na watamkabidhi Mzee Mpili