Siku ya Mkutano Mkuu wa Wananchama ambao ulifanya marekebisho ya Katiba kuruhusu Mabadiliko, Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Mhandisi Hersi Said aliweka hadharani ahadi iliyotolewa na Mwenyekiti wa Makampuni ya GSM, Ghalib Said Mohammed kuelekea msimu ujao
Katika usajili, GSM aliahidi kusajili wachezaji wa daraja la juu kuifanya Yanga iwe na ushindani sio hapa Tanzania tu bali ukanda wote wa Afrika
Tayari tumeshuhudia usajili wa mlinzi wa Kimataifa wa DR Congo ambaye alikuwa nahodha wa AS Vita, Shabani Djuma
Djuma alikuwa na akiwaniwa na timu kama Mamelodi Sundowns na hata Al Ahly usajili wake ukitajwa kugharimu zaidi ya Tsh Milioni 800
Imeelezwa huo ni mwanzo tu, kwani usajili wa nyota wa Kimataifa utatikisa nchi
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Athuman Kihamia amesema Wananchi wanapaswa watulie kwani mambo ndio kwanza yanaanza
"Watu wasidhani huyu Ghalib amekuja kujaribu Yanga, amedhamiria kweli, akiahidi huwa anatekeleza bila wasiwasi na subirini kishindo cha usajili, kuna mastraika wakubwa wenye rekodi wanakuja hapa Yanga siku sio nyingi," alisema KihamiaΒ
Aidha tayari GSM ameshusha basi la kisasa lenye thamani ya zaidi ya Tsh Bilioni Moja na pengine kuifanya Yanga kuwa klabu inayotumia mabasi ambayo wengi wamezoea kuyaona kule mamtoni yakimilikiwa na klabu kama Real Madrid, Liverpool n.k
Juzi kulikuwa na hafla maalum ambayo iliandaliwa na GSM, ambapo pamoja na mambo mengine, bilionea huyo alitimiza ahadi yake kwa kukabidhi 'mzigo' kwa wachezaji baada ya ushindi dhidi ya Simba