Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Injinia Hersi Said amesema pamoja na kuumizwa na matokeo ya mchezo wa fainali kombe la Shirikisho dhidi ya Simba, wamekubali matokeo, wanajipanga kuelekea msimu ujao
Yanga imepoteza mchezo kwa kufungwa bao 1-0 na Simba katika mchezo uliopigwa uwanja wa Lake Tanganyika, mkoani Kigoma
Injinia Hersi amesema wanajivunia wachezaji wote kwani walipambana kwa nguvu zote lakini bahati haikuwa upande wao
"Nasikitika kwamba tumepoteza mchezo wa fainali. Lakini nawapongeza wachezaji wetu kwa kupambana licha ya changamoto walizokumbana nazo"
"Tuna timu nzuri, sisi viongozi tunajivunia wachezaji hawa, wamejitoa kwa ajili ya timu yetu tangu tulipoanza msimu huu. Tunajipanga ili tuweze kuwa imara zaidi msimu ujao," alisema Injinia Hersi
Yanga imemaliza msimu ikiwa na taji moja la Mapinduzi waliloshinda visiwani Zanzibar kwa kuifunga Simba kwenye mchezo wa fainali
Aidha Wananchi watakuwa na mapumziko ya siku chache kabla ya kuelekea katika michuano ya kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza wiki ijayo jijini Dar es salaam