Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Haji Mfikirwa amesema wana matumaini makubwa kuwa watashinda shauri lao dhidi ya mchezaji Bernard Morrison kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS)
Shauri la Yanga dhidi ya Morrison litasikilizwa na Mahakama hiyo kuanzia keshokutwa Alhamisi, Julai 29 2021
Mfikirwa amesema kesi hiyo itasikilizwa kwa haki na wanaamini maamuzi yatatolewa kwa haki pia
"Kama ambavyo CAS wametangaza kesi itasikilizwa tarehe 29, maamuzi yanabaki kwao lakini kwetu sisi hatuna wasiwasi kwa sababu tuna uhakika wa kushinda," alisema Mfikirwa
Morrison anatuhumiwa kusaini mkataba na Yanga kisha kuukana mkataba huo na kwenda kusajiliwa na Simba
Katika hukumu yake, Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ilibaini Morrison alisaini mkataba na Yanga lakini ikadai ulikuwa na mapungufu na hivyo kumtangaza kuwa ni mchezaji huru
Hata hivyo shauri lililokuwa limepelekwa mbele ya Kamati hiyo ilikuwa kubaini kama Morrison alikuwa amesaini mkataba na Yanga au la baada ya mwenyewe kudai hakuwa amesaini mkataba licha ya pia kuthibitishwa kuwa alichukua fedha za Yanga dola 30,000 ambazo aliagizwa azirudishe