Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema ukizungumzia klabu yenye thamani kubwa hapa Tanzania, Yanga itakaa kwenye nafasi ya kwanza
Jana Mwekezaji wa Simba Mohammed Dewji alisema klabu yake haiwezi kupewa udhamini unaolingana na Yanga kwa kuwa timu yao ni kubwa pamoja na kuwa na mashabiki wengi
Ni kauli iliyoibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii, Bumbuli akiwa miongoni mwa waliotoa maoni yao
"Yanga ndio klabu yenye thamani kubwa kwenye Soka la Tanzania, sisi tunaweza kuendesha hafla au shughuli yetu bila kuzungumzia timu nyingine yoyote Duniani, bila kujitapa na bila kurusha kijembe chochote kwa mtu wala timu yoyote"
"Wengine sasa, wanalazimisha ukubwa wa brand kwa kuitaja Yanga kila tukio lao," aliandika Bumbuli kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii
Aidha Bumbuli aliwapiga dongo Simba kuwa fedha ambazo Yanga wataingiza kutokana na mkataba wa maudhui waliosaini na Azam Media, zinatosha kuinunua klabu hiyo
"Tulisaini Mkataba wa Bil 34.8 ambazo sisi Yanga tunazipata. Kwa hiyo tunaweza kuandika bango kama lile walilokabidhiwa, kisha tukawapa halafu tukamiliki asilimia zetu kwao"
Yanga ilisaini mkataba na Azam Media wenye thamani ya Tsh Bilioni 41 (pamoja na VAT) ambapo Yanga itavuna hadi Tsh Bilioni 4 kwa mwaka
Fedha hizo ni mara mbili ya fedha za uwekezaji ambazo Mo amelipa kununua hisa asilimia 49 katika klabu ya Simba
Kwa Yanga hizo Bil 41 ni fedha za Mkataba mmoja tu wa Maudhui na Azam Media. Bado hawajazungumzia fedha watazoingiza kutokana na mauzo ya hisa asilimia 49 zitakazonunuliwa na Wawekezaji watatu au wanne pale mchakato utakapokamilika
Taarifa za ndani zimebainisha kuwa Makadirio ya thamani ya Yanga ni Tsh Bilioni 200!
Ukubwa wa 'brand' haupimwi kwa mafanikio ya muda mfupi, Yanga ndio bingwa wa kihistoria hapa Tanzania ikikusanya mataji 27 ya ligi kuu
Ni timu iliyojijenga kwa miaka mingi, kwani mafanikio yamekuwa sehemu yao wakati wote
Zipo nyakati za mpito kwa kila timu. Ndio maana hata timu kama Manchester United ndio klabu yenye thamani kubwa zaidi kule Uingereza
Lakini ubingwa wao wa mwisho ligi kuu ya Uingereza ni msimu wa 2012/13!