Kocha Jackson Mayanja raia wa Uganda ambaye amewahi kuzinoa klabu za Simba, KMC, Coastal Union na Kagera Sugar, amepongeza usajili wa kiungo Khalid Aucho akiamini kuwa kiungo huyo atawasaidia Yanga kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mayanja ambaye pia amewahi kuwa nahodha wa Uganda Cranes, amesema anamfahamu vizuri Aucho, mchezaji wa timu ya Taifa ya Uganda
"Ni mchezaji mzuri. Ana uzoefu na ana nguvu pia, Yanga imepata mchezaji mzuri na anaichezea timu ya Taifa ya Uganda.
Nadhani watu wengi hasa Watanzania walimuona kwenye AFCON iliyopita na bado yupo timu ya taifa," alisema Mayanja.
Alisema uwapo wake kwenye kikosi cha Yanga utakuwa ni faida pia kwa timu yao ya taifa, kwani changamoto atakazokuwa akizipata, zitamfanya kuzidi kuongezeka ubora na kuisaidia nchi yao.
"Kwa sisi Waganda tunafarijika kwa sababu Lwanga yupo Simba na sasa Aucho atakuwa Yanga. Watakuwa wanaonyeshana ufundi. Na hii itakuwa si faida kwa timu hizo tu, bali hata kwa timu ya Taifa ya Uganda," alisema
Aucho alitua nchini kukamilisha usajili wake na Yanga mapema wiki ambapo jana aliondoka kurejea kwao Uganda kukamilisha masuala yake binafsi kabla ya kuelekea kambini na kikosi cha Yanga nchini Morocco