Jana Rais wa TFF Wallace Karia alitangaza kuruhusu klabu kusajili wachezaji 12 wa kigeni kwa ajili ya michuano mbalimbali msimu ujao
Katika hao 12, watakaoruhusiwa kutumika katika mchezo mmoja ni wachezaji nane tu
Karia alitaja miongoni mwa sababu iliyopelekea marekebisho ya kanuni hiyo ni baada ya CAF kuongeza idadi ya wachezaji katika michuano yao kutoka 30 hadi 40 kutokana na changamoto ya corona
Hivyo maboresho ya kanuni hiyo yamelenga kuzisadia timu zitakazoshiriki michuano ya CAF kushiriki michuano hiyo na wachezaji 12 wa kigeni
Hata hivyo cha kushangaza uamuzi huo umetangazwa siku moja kabla ya dirisha la usajili kwa ajili ya michuano ya CAF kufungwa
Na wakati huohuo ni timu moja tu (Simba) inayoonekana kuwa ilisajili wachezaji zaidi ya 10 mapema, ni kama walifahamu mabadiliko hayo
Azam Fc walishafunga usajili wao na nyota 10 wa kigeni, Yanga wametangaza kukamilisha usajili wa wachezaji 10 wa kigeni, Biashara United nao wana nyota kadhaa wa kigeni
Wakati mwingine TFF wanajiweka katika mazingira ya kulaumiwa kuwa wanaibeba Simba kutokana na maamuzi ya aina hiyo
Kama walikuwa wanataka timu zote zinufaike na Mabadiliko ya kanuni hiyo, basi walipaswa kutangaza Julai 19 siku ambayo walifungua dirisha la usajili
Hapa inaonekana ni timu moja iliyosajili wachezaji 12 au zaidi, na ndio iliyokwenda kuomba Mabadiliko ya kanuni hiyo TFF
Kwani sio Yanga, Azam Fc wala Biashara United iliyosajili zaidi ya wachezaji 10 wa kigeni
Lakini timu hizi pengine nazo zingependa kusajili wachezaji 12 ili kunufaika kwenye michuano ya Kimataifa lakini zimearifiwa siku moja kabla ya dirisha la usajili kufungwa
Hivyo hawawezi kusajili sasa pengine wakifanikiwa kutinga hatua ya makundi wanaweza kunufaika na kanuni hiyo. Kama watasajili baada ya leo na kabla ya August 31, wachezaji hao watatumika michuano ya ndani tu
Ukweli ni kwamba walioomba Mabadiliko hayo pengine walikuwa tayari wamesajili wachezaji hao 12 na kuona kanuni ya wachezaji 10 inawabana
Kwa upande mwingine idadi ya wachezaji 12 wa kigeni ni wengi sana. Haiwezi kuwa fahari timu kutoka Tanzania ikitwaa ubingwa wa Afrika ikiwa wachezaji wote 11 ni wa kigeni!
Nchi zilizofanikiwa sana katika soka barani Afrika, idadi ya nyota wa kigeni hawazidi watano. Tanzania ndio nchi inayoruhusu idadi kubwa ya nyota wa kigeni
Kusema nyota hawa wa kigeni wanakuja kuwapa changamoto wachezaji wa ndani ili kuimarisha viwango vyao sio kweli
Wachezaji wanaotoka nje wanasajiliwa kwa gharama kubwa, hawa wanalazimika kuwa chaguo la kwanza kikosini hata kama viwango vyao havitofautiani sana na wazawa
Wakati mwingine makocha wanawekwa kwenye presha kubwa na viongozi kuwatumia wachezaji wa kigeni ili kukwepa lawama za mashabiki kutokana na gharama iliyotumika kuwasajili
Athari ya maamuzi haya itaonekana kwenye timu ya Taifa kwani asimilia 90 ya wachezaji wanaochaguliwa hutoka katika klabu za Yanga, Simba na Azam Fc ambazo zimesajili wachezaji 12 wa kigeni!
Wengi wa wachezaji hawapati nafasi za kucheza mara kwa mara na hivyo kukosa uzoefu unaohitajika kufanya vizuri kwenye michuano ya Kimataifa