Rais wa Makampuni ya GSM Ghalib Said Mohammed ameungana na wadau wengine wa soka nchini kumchangia mchezaji wa Polisi Tanzania Gerrard Mdamu ambaye alivunjika miguu yote miwili katika ajali mwishoni mwa msimu uliopita
Galib ametoa Tsh Milioni sita, fedha ambazo ziliwasilishwa kwa niaba yake na Msemaji wa Yanga Haji Manara
Aidha, Manara nae akatoa mshahara wake wa mwisho aliolipwa na Simba (Tsh 700,000/-) na hivyo kuwasilisha Tsh Milioni 6.7

Katika mahojiano na Wasafi Fm mapema leo, Manara alimtaja Ghalib kama mtu wa watu mwenye moyo wa kusaidia wengine pasipo kujionyesha
"Ghalib ni mtu wa watu na kama wengine walivyojitokeza kumchangia Gerald Mathias Mdamu ambaye ni mchezaji wa Polisi Tanzania nae pia ameguswa na kutoa mchango wake wa pesa milioni 6 ambapo tutaukabidhi sehemu husika"
"Pia nami natoa mshahara wangu wa mwezi wa saba ambao ni shilingi laki saba ili kusaidia matibabu ya kijana huyu. Yanga tunaahidi kuwa bega kwa bega kuhakikisha ndoto za Mdamu hazifi, tutaendelea kumshika mkono na tunaomba wengine kumchangia ili afanikishe matibabu," alisema Manara