Saa 11 jioni Wananchi watashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kuiwakilisha nchi katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, hatua ya awali wakiwakabili Rivers United kutoka Nigeria
Ni mchezo unaosuburiwa kwa hamu na mashabiki wa Yanga, nchi nzima itakuwa mbashara Azam Sport 1 ifikapo saa 11 jioni kwani mchezo utachezwa bila ya mashabiki uwanjani
Hakuna matokeo mengine tofauti na ushindi ambayo kikosi cha kocha Mohammed Nasreddine Nabi kinahitaji kuyapata ili kwenda Nigeria katika mchezo wa marudiano wakiwa kifua mbele
Habari njema ni kuwa kikosi cha Nabi kiko kamili pamoja na changamoto ya kuwakosa baadhi ya wachezaji waliokuwa na shida katika ITC zao
Shabani Djuma, Khalid Aucho na Fiston Mayele ndio wachezaji wanaokosekana baada ya ITC zao kuchelewa
Aidha Mapinduzi Balama yeye anaendelea kuimarika wakati Yassin Mustafa aliyerejea kikosini karibuni nae huenda asiwe sehemu ya mchezo kwa sababu bado hayuko fit kwa asilimia 100
Kwa wale watakaopewa nafasi ya kucheza leo, wafahamu kuwa wanabeba matumaini ya mamilioni ya Watanzania mashabiki wa Yanga ambao wanahitaji furaha