Jana Yanga ilipoteza mchezo muhimu wa ligi ya mabingwa nyumbani kwa kufungwa bao 1-0 na Rivers United katika mchezo uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Ni matokeo yaliyowaumiza mashabiki wa Yanga hadi wengine kufikia kuhoji maamuzi ya kocha Nasreddine Nabi kuwaweka nje baadhi ya wachezaji huku wengine wakihoji aina ya 'sub' alizofanya kwenye mchezo huo
Wakati mchezo huo ukielekea ukingoni, Nabi aliwaingiza Yusufu Athumani kuchukua nafasi ya Heritier Makambo aliyekuwa amepata jeraha huku Saido Ntibazonkiza akiingia kuchukua nafasi ya Zawadi Mauya
Mapema alimuingiza Ditram Nchimbi kuchukua nafasi ya Yacouba Songne
Saido alionekana kuwa na mchango mkubwa katika dakika chache alizocheza kupelekea wengi kuhoji kwa nini hakutumika tangu mapema?
Akizungumza na Wanahabari baada ya mchezo, Nabi alisema kwake yeye aliyebadili mchezo ni Yusufu na alikuwa na sababu za msingi kutomuingiza Saido mapema
"Yusufu (Athumani) ndiye aliyebadili mchezo, kuingia kwake kulikuwa na faida zaidi kwenye safu ya ushambuliaji sio Saido"
"Saido anacheza nafasi ambayo yupo Fei Toto je kama wewe ni kocha unaweza kumtoa Fei Toto umuingize Saido?"
"Kutokana na sababu za umri, Saido hawezi kucheza dakika 90, mchezo ulihitaji vijana wanaoweza kufanya majukumu mengi uwanjani," alisema Nabi
Aidha alitaja sababu ya msingi iliyopelekea timu yake isipate matokeo mazuri katika mchezo huo kuwa ni maandalizi hayakuwa ya kutosha
"Hatukuwa na muda wa kutosha kufanya mazoezi pamoja, tunayo timu nzuri na tunaweza kwenda kupata matokeo Nigeria"
Nabi amelaumiwa na wengi kwa aina ya kikosi alichotumia katika mchezo huo muhimu nyumbani
Kutowatumia wachezaji wazoefu kama Yannick Bangala pamoja na kufanya mabadiliko ya kumtoa Yacouba Songne na kumuingiza Ditram Nchimbi ni miongoni mwa maamuzi yaliyowashangaza wengi