Kocha wa zamani wa Yanga Mwinyi Zahera, amesema mabingwa hao kihistoria wana nafasi ya 'kupindua meza' Nigeria kwa kupata ushindi dhidi ya Rivers United
Zahera anayetarajiwa kuwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya soka la Vijana, amewahi kupindua meza ugenini wakati akiwa kocha msimu wa 2019/20 kwenye michuano ya ligi ya mabingwa
Kikosi chake kililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Township Rollers jijini Dar es salaam na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kule Botswana na kutinga raundi ya kwanza
Zahera amesema licha ya kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani, nafasi bado ipo kwa Yanga kupata ushindi ugenini
"Nafasi ya Yanga kusonga mbele michuano ya ligi ya mabingwa ipo. Wale Rivers United wanafungika vizuri tu kama wachezaji watakuwa makini kwenye ushambuliaji na eneo la kiungo"
"Yanga hawapaswi kupoteza sekunde hata moja ya muda, washambulie muda wote wa dakika 90 wajue jukumu lao na wawepo uwanjani kwa timu nzima pia," alisema Zahera
Yanga itaondoka keshokutwa Ijumaa kwa ndege ya kukodi kwenda moja kwa moja Nigeria na timu itarejea nchini siku hiyohiyo ya Jumapili baada ya mchezo
Msafara utajumuisha mashabiki takribani 48 ambao watapata fursa ya kuishangilia timu itakapokuwa dimbani kule Nigeria