Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga ambaye pia amewahi kuwa mchezaji na kocha wa mabingwa hao wa kihistoria, Charles Mkwasa amesema kimahesabu Yanga ina nafasi ya kusonga mbele michuano ya ligi ya mabingwa kama itaifunga Rivers United
Hata hivyo amesisitiza ni muhimu kocha Nasreddine Nabi kukiimarisha kikosi chake ili wachezaji watumie kila nafasi itakayopatikana katika mchezo huo utakaofanyika Septemba 19, katika Uwanja wa Yakubu Gowon huko Nigeria
Yanga inashuka dimbani katika mchezo huo ikiwa nyuma kwa bao 1-0, baada ya kupoteza katika mchezo wa kwanza uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Jumapili iliyopita
Mkwasa amesema kuwa Yanga, inakabiliwa na mchezo mgumu unaohitaji matokeo ya ushindi ili iweze kusonga mbele na itawezekana kama umakini utaongezeka hasa katika safu ya ulinzi ipunguze makosa na safu ya ushambuliaji itumie kila nafasi itakayopatikana.
"Bado kuna nafasi kwao ya kusonga mbele ila wanapaswa kufanya kazi kubwa lakini kama watatulia na kuhakikisha wanatumia kila nafasi wanayoipata naamini hilo litazaa matunda, Yanga itashinda." alisema Mkwasa
Yanga itaondoka nchini kesho Ijumaa kwa usafiri wa ndege ya kukodi (ATCL) na itarejea siku ya Jumapili baada ya mchezo