Mlinzi wa kushoto wa Yanga David Bryson alianza mazoezi ya timu mwanzoni mwa wiki hii baada ya kupona majeraha yaliyomuweka nje kwa wiki kadhaa
Juzi Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi alimtumia Bryson katika mchezo wa kirafiki dhidi ya DTB na akafanikiwa kufunga bao moja katika ushindi wa mabao 3-1 ambao Yanga waliupata
Kiwango alichoonyesha Bryson kimempa matumaini Nabi kuelekea mchezo Ngao ya Jamii dhidi ya Simba utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi
Nabi amesema Bryson alikuwa bora katika mchezo huo ambao alicheza kwa dakika zote 90
"Ni jambo jema amerejea uwanjani akiwa katika kiwango kizuri sana, anakuja kuongeza ushindani wa namba kikosini, ninahofu tu kwamba pengine hajawa fiti asilimia zote kwa sababu amekuwa nje kwa muda mrefu lakini kwake hili naona haliko akilini hivyo ananipa matumaini sana," Nabi aliiambia tovuti ya Yanga
Tangu mwezi April, Yanga imemtegemea zaidi Adeyum Saleh baada ya Yassin Mustafa kupata majeraha
Wakati mwingine Nabi alilazimika kumtumia Kibwana Shomari katika safu ya ulinzi upande wa kushoto pale Adeyum alipokosekana
Kama Nabi ataridhishwa na utimamu wa Bryson kuelekea mchezo wa Jumamosi, pengine anaweza kupewa nafasi
Kama sivyo, huenda Kibwana akaanza upande wa kushoto huku Shabani Djuma akicheza namba 2