Msemaji wa klabu ya Yanga Haji Manara amesema baada ya kufanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii, wamedhamiria pia kushinda ubingwa wa ligi kuu, kutwaa taji la Shirikisho la Azam (ASFC) na kombe la Mapinduzi, hivyo kila mchezo watakaoshuka dimbani kucheza ni fainali
Manara ni mmoja wa viongozi wa Yanga ambao watakuwa na timu mkoani Kagera kuhakikisha alama zote tatu zinapatikana katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi ambao utapigwa dhidi ya Kagera Sugar kesho katika uwanja wa Kaitaba
Amesema msimu huu hawahitaji kulalamika, wanataka kuona kila mchezo wanapambana kwa nguvu zote kuhakikisha wanapata matokeo
"Sisi ndio mabingwa wa kihistoria, mabingwa mara 27 ligi kuu, tunaposema The Return of Champions tunamaanisha. Tunataka kushinda makombe yote msimu huu, tumeanza na Ngao ya Jamii. Tunakwenda kupambana katika kila mchezo kuhakikisha tunapata matokeo, mchezo wetu wa kwanza ni dhidi ya Kagera Sugar"
"Sisi hatutalalamika safari hii kwani tunaamini, Bodi ya Ligi, TFF pamoja na Waamuzi watasimia haki, jukumu letu ni kuhakikisha tunashinda kila mchezo. Mechi yoyote inayokuja mbele yetu ni fainali ambayo lazima tushinde," alisema Manara
Yanga ilitua Bukoba jana, ambapo jioni Wananchi walianza maandalizi kuelekea mchezo huo muhimu