Kocha wa Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema anafurahi kuona timu yake ikiendelea kuimarika siku baada ya siku licha ya kupata ushindi mwembamba kwenye mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara walizocheza hivi karibuni
Yanga ilipata ushindi wake wa pili juzi kwa kuifunga Geita Gold bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kujikita katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi nyuma ya vinara Polisi Tanzania, zote zikiwa na pointi sita zikitofautiana kwa mabao ya kufunga
Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Geita FC, Nabi alisema inaridhisha kuona timu ikizidi kuimarika katika kila mechi walizocheza na hiyo inampa matumaini ya kufanya vizuri zaidi kwenye ligi hiyo
"Niwapongeze wachezaji kwa ushindi wa pili mfululizo kwenye ligi, mchezo ulikuwa mzuri kwa timu zote mbili lakini tulistahili kupata ushindi kutokana na kiwango ambacho tulikionesha, tumeonesha ubora halisi wa timu nitakayokuwa nayo msimu huu," alisema Nabi
Kocha huyo raia wa Tunisia alisema anapambana kuongeza utimamu wa mwili pamoja na umaliziaji kwa wachezaji wake kwani imekuwa tatizo katika mechi walizocheza.
Alisema wakati wa mapumziko mafupi ya ligi kwenye kambi ya muda mfupi watakayoweka mkoani Arusha, anaamini itampa nafasi kurekebisha kasoro zote