Kocha Mkuu wa Yanga Nasriddine Nabi amesema licha ya washambuliaji wake kuanza msimu kwa kusuasua, lakini imani yake juu yao ni kibwa
Katika mechi mbili za ligi kuu ambazo Yanga imecheza imefunga mabao mawili na yote yamefungwa na viungo na siyo washambuliaji wake tegemezi Fiston Mayele na Heritier Makambo.
Nabi amesema hana shaka na uwezo waliokuwa nao wachezaji hao ispokuwa ugeni wa ligi ndio unawasumbua ingawa baada ya muda mfupi kila kitu kitakaa sawa kwao.

"Hawa ni washambuliaji wa viwango kila mtu anajua hilo sababu walishathibitisha ubora wao tangu huko walikokuwa sasa kutofunga mabao kipindi hiki hakiwezi kuwa sababu ya kuwaona hawafai kinachowakuta mchezaji yeyote duniani kinaweza kumtokea hivyo mashabiki wawe watulivu," amesema Nabi
Kocha huyo amesema kitu kingine kinachosababisha wachezaji hao kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo ni kukutana na wachezaji tofauti na wale ambao wamezoeana nao hivyo bado hawajaelewana vizuri
Mayele amejiunga na Yanga msimu huu akitokea AS Vita ya DR Congo na mpaka sasa amefunga bao moja kwenye mechi ya Ngao ya Jamii huku pia akifunga mabao matano katika michezo ya kirafiki
Makambo alifunga bao kwenye mchezo wa wiki ya Mwananchi dhidi ya Zanaco, bado hajaweza kuzifumania nyavu kwenye michezo ya mashindano