Mtendaji Mkuu wa klabu ya Yanga Senzo Mazingisa amesema waliuanza msimu taratibu lakini wameendelea kuimarika kila siku
Senzo amesema matokeo mazuri wanayopata sasa sio bahati, ubora unaonekana uwanjani
Yanga iko kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya mechi tatu, ikishinda mechi zote na kufunga mabao manne pasipo kuruhusu bao
"Nafikiri waliokuwa na wasiwasi na Yanga hii watagundua kwamba kikosi chetu kipo katika ubora mkubwa, hatushindi kwa kubahatisha tunaonyesha ubora mkubwa ndani ya uwanja," Senzo amenukuliwa na gazeti la Mwanaspoti
"Timu imefunga mabao manne katika mechi tatu na mabao hayo yamefungwa na washambuliaji na viungo lakini ukiangalia hata safu ya kiungo inatengeneza nafasi vizuri bila presha hii ndio timu ambayo tunaitaka"
"Hatujaruhusu bao mpaka sasa, kuna ubora ambao wanao walinzi wetu, angalia kipa wetu Diarra (Djigui) na mabeki wote, nafikiri kuna heshima ambayo tunastahili kupewa mtu anapoizungumzia Yanga na sio kuona kama tunabahatisha"
"Tuna tofauti ukiangalia hata msimu uliopita tulianza ligi kwa kasi kubwa lakini baadaye mwishoni tukapungua kasi tukakosa ubingwa, msimu huu tofauti tumeanza taratibu kidogo na kulikuwa na sababu ila muda unavyosogea tunazidi kuwa bora zaidi," aliongeza Senzo