Baada ya mapumziko ya siku mbili, kikosi cha Yanga kinarejea kambini leo kuendelea na maandalizi ya mchezo wa ligi kuu unaofuata dhidi ya Namungo Fc
Mchezo huo utapigwa Novemba 20 kwenye uwanja wa Ilulu, Lindi
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema baadhi ya wachezaji wanatarajiwa kuondoka leo kwenda kujiunga na timu za Taifa
Nyota watatu wa kigeni Khalid Aucho, Yacouba Songne na Djigui Diarra wamejumuishwa katika timu za Taifa za Uganda, Burkina Faso na Mali
Aidha Ramadhani Kabwili, Kibwana Shomari, Bakari Nondo Mwamnyeto, Dickson Job, Zawadi Mauya na Feisal Salum wamejumuishwa kwenye timu ya Taifa ya Tanzania ambayo itaingia kambini keshokutwa kujiandaa na mchezo dhidi ya DR Congo
"Wachezaji watatu wa kigeni Aucho, Diarra na Yacouba wanaondoka leo kujiunga na timu zao za Taifa wakati wale walioitwa kwenye timu ya Taifa ya Tanzania watarudi kambini kabla ya kwenda kujiunga na timu ya Taifa Jumamosi"
"Wachezaji wengine wote wataendelea na maandalizi ya mchezo dhidi ya Namungo Fc, " alisema Bumbuli