Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Steven Mguto amesema kitendo cha kuhusisha udhamini wa Soka na kupanga matokeo ni sawa na kuwakosea heshima wanaojitolea fedha zao kuboresha mazingira ya soka nchini
Wiki iliyopita kuliibuliwa mjadala na baadhi ya wanahabari waliokuwa wakihoji hatua ya GSM kudhamini timu zaidi ya moja
Mguto amesema kwenye kanuni za uendeshaji wa ligi hakuna kipengele kinachomzuia Mdhamini kudhamini zaidi ya timu moja
Amesema jambo hilo sio kosa na si vyema kulihusisha na masuala ya upangaji wa matokeo
"Katika kanuni zetu sio kosa kwa mdhamini mmoja kudhamini timu zaidi ya moja. Ieleweke kuna tofauti kubwa kati ya kupanga matokeo na kudhamini timu zaidi ya moja"
"Kutolea mfano udhamini kama sehemu ya upangaji wa matokeo ni kuwakosea heshima waliojitolea fedha zao kuokoa soka letu," alisema Mguto
Wadau mbalimbali wa soka wamekosoa mijadala hiyo iliyoibuliwa na kundi la wanahabari ambao wengi wanaamini uliibuliwa makusudi wakati huu ambao udhamini wa GSM kwa klabu ya Yanga umekuwa na mafanikio
Yanga imeshinda mechi zote tano za ligi kuu msimu huu ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi na alama 15