Kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wa Yanga katika mechi za kirafiki walizocheza visiwani Zanzibar, kimemuongezea imani kocha Nasreddine Nabi ambaye sasa anaamini timu yake imeiva
Yanga ilialikwa Zanzibar kwenye maadhimisho ya mwaka mmoja wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi ambapo ilicheza mechi mbili na kufanikiwa kushinda mechi zote
Katika michezo hiyo dhidi ya Mlandege na KMKM Yanga iliwakosa wachezaji wake 14 ambapo 10 walikuwa na majukumu ya timu za Taifa huku wanne wakiwa majeruhi
Nabi ameeleza kufurahishwa na ubora ulioonyeshwa na wachezaji wake akiamini ushindani utaongezeka pale waliokuwa na majukumu ya timu za Taifa watakaporejea
"Nimefurahishwa na wachezaji waliokuwa katika kambi Zanzibar kwani wamepambana kwa kuonyesha wanastahili kupewa nafasi ya kucheza katika mechi za ushindani hili ni jambo jema kwetu," alisema Nabi
"Jambo hilo litaongeza ushindani katika timu lakini hakutakuwa na tofauti kubwa kati ya wale ambao wanapata nafasi ya kuanza na watakaokuwa benchi kila ambaye atapata nafasi atafanya kazi yake ipasavyo"
Yanga ilirejea Dar es salaam mwishoni mwa wiki ambapo leo imeanza maandalizi ya mchezo dhidi ya Namungo Fc ambao utapigwa Jumamosi, Novemba 20 kwenye uwanja wa Ilulu, Lindi