Kikosi cha Yanga majira ya saa 10 jioni kitashuka kwenye uwanja wa Sokoine kuikabili Mbeya Kwanza ukiwa ni mwendelezo wa ligi kuu ya NBC, raundi ya 7
Vinara hao wa ligi wamepania kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi wakizihitaji alama zote tatu
Yanga wako mkoani Mbeya tangu juzi Jumapili wakijiandaa na mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali
Mbeya Kwanza ni miongoni mwa timu zilizoanza vyema msimu huu ikiwa imefungwa mchezo mmoja, wameshinda mmoja na kutoka sare michezo minne. Wamekuwa wagumu kufungika wanapokuwa nyumbani
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi leo anatarajiwa kufanya mabadiliko ya kikosi chake baada ya kuwakosa baadhi ya wachezaji kutokana na sababu mbalimbali
Kiungo Yannick Bangala anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano huku wachezaji Jesus Moloko na Yacouba Songne wakiwa ni majeruhi
Aidha Nabi anaweza kumpumzisha kiungo Khalid Aucho ambaye amerejea kikosini hivi karibuni baada ya kupona majeraha aliyopata wakati akiitumikia timu ya Taifa
Aucho pia ana kadi mbili za njano, ipo hatari ya kuukosa mchezo dhidi ya Simba kama atacheza na kupewa kadi ya njano leo
Nabi amesema atatoa nafasi kwa wachezaji wengine kuonyesha uwezo wao akiamini wataondoka mkoani Mbeya na alama zote tatu