Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema hapo kesho dakika 90 zitaamua matokeo ya mchezo wa ligi kuu kati ya Simba dhidi ya Yanga ambao utapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11 jioni
Nabi ambaye kikosi chake cha Yanga kinaongoza ligi kikiwa na alama 19 baada ya kushuka dimbani mara saba, amesema yeye hana maneno mengi kama walivyo makocha wengine lakini kazi yake itaonekana uwanjani
Amesema ameiandaa timu yake vizuri akiwataka mashabiki wa Yanga wajitokeze kwa wingi kushuhudia mchezo mzuri kutoka kwa timu yao
"Mimi ni mtu wa mpira na sipendelei sana manenomaneno zaidi ya kufanya kazi, unajua kila mtu anafanya vizuri katika kitu ambacho anakipenda na anakijua hivyo mimi ni mtu wa mpira"
"Wapinzani wetu nawaheshimu na nimewaona namna ambavyo wanacheza ni jambo la kusubiri na kuona itakuaje lakini ninachoweza kusema ni kwamba tupo tayari, " amesema
"Utakuwa mchezo mzuri, mashabiki wetu waje kwa wingi uwanja, sisi tuko tayari kuwapa burudani"
Nabi ameiongoza Yanga katika michezo mitatu dhidi ya Simba akishinda miwili na kupoteza mchezo mmoja
Mchezo wa Jumamosi utakuwa wa nne, matokeo ya ushindi ni muhimu kwa Yanga ili kuzidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi katika mbio za kuwania ubingwa