Ilikuwa ni miezi, wiki, siku na hatimaye saa chache kutoka sasa, mchezo mkubwa zaidi katika ligi ya NBC unaozikutanisha timu zenye upinzani wa kihistoria Yanga na Simba, unapigwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Siku ya leo ifikapo majira ya saa 11 jioni, shughuli nyingi zitasimama kupisha mchezo huo
Ni dabi ambayo inaweza kuwa tofauti kidogo kulinganisha na michezo minne ya aina hiyo iliyopigwa kabla
Wakati huu Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikionekana kuwa imara zaidi huku wapinzani wao wakionekana kushuka kiwango
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo, alisema wengi wanaipata nafasi Yanga kushinda lakini yeye anaamini timu zote zina nafasi sawa (50/50)
Ugumu wa mchezo unatokana na ukweli kuwa matokeo yake yanaweza kuwa na athari ya moja kwa moja kwa wachezaji na makocha
Timu inayoshinda itanufaika kutokana na bonasi kubwa wanazopata kutoka kwa wadhamini wao lakini timu inayopoteza wachezaji na makocha wake wanaweza kujikuta matatani
Afisa Mhamasishaji wa Yanga Haji Manara amesema wataingia kwenye mchezo huo kwa lengo la kuibuka na ushindi lakini jambo muhimu ni kuwa watawaheshimu wapinzani wao
Matokeo ya ushindi yataifanya Yanga iendelee kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi na pia itakuwa faida kwao katika kinyan'ganyiro cha kuwania ubingwa wa ligi kuu
Yanga tayari wamechukua alama tatu kwa Azam Fc, wanazihitaji alama tatu dhidi ya Simba ili kuwa na faida mbele ya wapinzani wake hao katika mbio za kuwania ubingwa