Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema kikosi chake kina kila sababu ya kushinda ubingwa wa ligi kuu msimu huu lakini bado ana kazi ya kufanya kuhakikisha timu inakuwa katika ubora anaotaka
Yanga imeanza vyema msimu ikishinda michezo sita na kutoka sare michezo miwili ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 20
Licha ya wengi kuona Yanga imeiva kutokana na soka safi la pasi wanalocheza, Nabi amesema bado anahitaji kuendelea kukiboresha kikosi chake
Kocha huyo mwenye uraia pacha wa Tunisia na Ufaransa, amesema kikosi chake kitakapofikia pale anapotaka,Β itakuwa ngumu kukosa ubingwa
"Kwa jinsi ambavyo ninataka timu yangu icheze, hakuna kitakachoshindikana kwangu kubeba ubingwa. Nafurahishwa na tulipofikia sasa lakini bado tuna kazi ya kufanya"
"Ninaamini hivi karibuni mashabiki wa Yanga watafurahia zaidi.Nafahamu Wanayanga wana hamu ya ubingwa baada ya kuukosa kwa miaka minne, wawe na subira kwani tunayo nafasi ya kushinda msimu huu," alisema Nabi