Bodi ya ligi kuu Tanzania (TPLB) Jana December 17, 2021, ilikutana na wenyekiti wa vilabu vya ligi kuu Tanzania bara (NBC) katika kujadili masuala mbalimbali yanayohusu udhamini wa ligi kuu msimu wa 2021/22
Katika kikao hicho viongozi wa Klabu hizo walipata nafasi ya kushauriana na kukubaliana na bodi ya ligi kuu kuhusu namna bora zaidi ya kutekeleza masharti ya mikataba ya udhamini kwa lengo la kuhakikisha wadhamini waliopo wanaridhishwa na utekelezaji lakini pia kuvutia wadhamini wapya.
Kuhusu suala la kampuni ya GSM Tanzania Limited ambae ni mdhamini mwenza wa ligi kuu ya NBC, Klabu 15 Kati ya 16 zinazoshiriki ligi hiyo zimetoka na azimio ya kuendelea kutekeleza matakwa ya mkataba huo ikiwemo kuweka nembo ya GSM kwenye bega la kushoto la Jezi zinazotumika kwa Michezo ya ligi kuu hiyo
Klabu hizo 15 (Geita Gold, Mtibwa sugar, Mbeya Kwanza, Tanzania Prisons, Biashara United, Ruvu Shooting, KMC FC, Kagera Sugar, Namungo FC, Azam FC, Coastal Union, Dodoma Jiji FC, Polisi Tanzania, Mbeya City na Yanga SC) zimeridhia na Utaratibu uliotumika katika kuingia mikataba yote ya udhamini msimu huu na wakiziomba bodi ya ligi na shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF),kuendelea na Juhudi za kutafuta wadhamini zaidi
Bodi ya ligi kuu inazishukuru Klabu zote zinazoshiriki ligi kuu ya NBC msimu huu kwa ushirikiano wao katika kujadili changamoto na kutafuta majibu kwa pamoja.
Bodi imezitaka Klabu kuendelea kutekeleza kikamilifu matakwa ya mikataba yote ya udhamini kwani jambo hilo huvutia pia wadhamini wapya
Katika hatua nyingine, Uongozi wa benki ya NBC na mwakilishi wa makampuni ya kutengeneza mabasi ya YuTong, wamezungumza na wenyekiti hao wa vilabu kuhusu Utaratibu wa kukopeshwa mabasi ya kisasa kwa ajiri ya safari ya timu zao
Klabu zilizo tayari kwa ajiri ya kukopa mabasi hayo, zimetakiwa kutuma barua bodi ya ligi ili mchakato huo ufanyike kupitia makubaliano kati ya NBC na TFF