Kiungo mpya wa Yanga, Salum Abubakary 'Sure Boy' amesema kujiunga na timu hiyo kuna maana kubwa kwake.
Aidha, amesema lengo lake kubwa kwa sasa ni kushirikiana na wachezaji wenzake ili kutimiza malengo ya klabu kubeba mataji yote msimu huu.
Sure Boy tayari ametambulishwa na Yanga baada ya kumalizana na timu yake ya Azam FC ambayo ameitumikia kwa zaidi ya misimu 14.
Sureboy amesema kuwa anafahamu Yanga ina ushindani mkubwa wa namba na nafasi anayocheza kuna wachezaji wengine bora na wanafanya vizuri lakini atapambana mazoezini ili kumshawishi kocha kumpa nafasi.
"Nimejiunga na timu yenye presha kubwa kuanzia malengo iliyonayo lakini pia kucheza Yanga unatakiwa kuwa fiti vinginevyo unaweza kujikuta unapotea, binafsi nimejipanga kukabiliana navyo vyote nikishirikiana na wachezaji wengine naamini tutafanikiwa," alisema Sure Boy
Kiungo huyo alisema asilimia kubwa ya wachezaji wa Yanga ni rafiki zake na huwa wanakutana timu ya taifa kwa hiyo hakuna ugumu kwake sababu mpira ni ule ule cha msingi ni kutekeleza kile anachoelezwa na kocha
Alisema anajisikia furaha kubadilisha mazingira na amejipanga kuhakikisha anatoa mchango wake ili kusaidia timu ifikie malengo ambayo imekusudia msimu huu