Jambo la uhakika ni kuwa Yanga inasubiri kutambulisha usajili wa winga Denis Nkane ambaye jana alicheza mchezo wake wa mwisho katika klabu ya Biashara United na kuwafungia bao lililowapa alama moja mbele ya Namungo Fc
Tangu msimu uliopita Yanga ilirejesha utamaduni wake wa kusajili mawinga wenye kasi ambao wanainufaisha timu wakitokea pembeni
Tuisila Kisinda alifanya vizuri kwenye msimu wake mmoja aliyoitumikia Yanga na kupata ofa nono kule RS Berkane
Wananchi wakamleta Jesus Moloko kuchukua nafasi yake na sasa kwenye usajili wa dirisha dogo wanamleta Nkane
Nkane ni moja ya sajili bora sana, wale wanaosema huyu 'dogo' hatafanikiwa Yanga, wakae kwa kutulia kwani huu mchezo hautaki hasira
Nkane ni toleo jipya la Mrisho Ngasa, wale waliomshuhudia Ngasa wakati akiwa kwenye ubora wake, basi ndivyo huyu Nkane alivyo sasa
Winga mwenye kasi na uwezo mkubwa wa kukimbia akiwa na mpira mguuni
Huyu sio winga wa kutengeneza mabao tu, lakini pia anafunga
Nkane anayo nafasi ya kuingia kwenye kikosi cha kwanza moja kwa moja hasa wakati huu ambao Yanga inaendelea kumkosa Yacouba Songne
Wananchi watamshuhudia katika michuano ya kombe la Mapinduzi inayoanza Januari 02 visiwani Zanzibar