Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema kikosi chake kimeshakamilisha maandalizi kuelekea mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha
Nabi amesema mechi ya kesho itakuwa tofauti kwa sababu zinakutana timu ambazo zimebadilisha wachezaji wake kwa asilimia kubwa tofauti na walivyokuwa msimu uliopita.
Kocha huyo alisema anajua wapinzani wao wamejipanga kuendeleza rekodi nzuri dhidi yao lakini wafahamu mpira wa Yanga umebadilika.
Alisema anafahamu mechi zote za ligi ni ngumu na Yanga imejiandaa kukabiliana na ushindani kwa ajili ya kufikia malengo ya kutwaa ubingwa msimu huu.
"Yanga hii ni tofauti, ni timu nyingine, ina wachezaji wapya, tunabadilika kulingana na aina ya mpinzani, nina matarajio utakuwa mecho mzuri lakini si rahisi," alisema Nabi
Aliongeza wachezaji wote walioko Arusha wako tayari kwa mechi hiyo na anafurahi kuona ushindani wa kuingia kwenye kikosi cha kwanza umeongezeka.
"Tuna kikosi kilichokamilika, kila mmoja ana nafasi ya kuanza, hili ni jambo jema kwa timu na inatusaidia katika kupanga kikosi, tumejiandaa kuendeleza kasi yetu"