Wananchi wako mkoani Arusha ambapo jioni ya leo watashuka uwanja wa Sheikh Amri Abeid kuikabili Polisi Tanzania katika moja ya michezo migumu ligi kuu ya NBC msimu huu
Historia ya timu hizi zinapokutana mara nyingi ushindani huwa ni mkubwa ambapo katika michezo minne ya iliyopita, Yanga imeshinda mchezo mmoja na michezo mitatu kumalizika kwa sare
Msimu uliopita Polisi Tanzania ni moja ya timu zilizovuruga mpango wa Yanga katika mbio za ubingwa baada ya Wananchi kulazimishwa sare ya bao 1-1
Yanga ilitoka mkoani Tanga ambako walifungwa na Coastal Union mabao 2-1. Sare ya Polisi Tanzania msimu uliopita ilipelekea uongozi wa Yanga kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu wakati huo Cedric Kaze ambaye sasa ni kocha msaidizi katika kikosi cha Nasreddine Nabi
Msimu huu Yanga imefanikiwa kuondoka na alama zote tatu dhidi ya Coastal Union na leo wanazihitaji alama tatu za Polisi Tanzania
Polisi Tanzania ni moja ya timu ngumu msimu huu ikishika nafasi ya tano wakikusanya alama 18
Wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama saba dhidi ya Simba inayoshika nafasi ya pili, ushindi kwa Yanga utawashuhudia mabingwa hao wa kihistoria wakiongeza utofauti wa pointi kuwa 10