Wananchi wameondoka na alama zote tatu mkoani Arusha baada ya kuichapa Polisi Tanzania bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid
Dickson Ambundo 'Super Sub' ndiye aliyeifungia Yanga bao pekee akifanya kazi nzuri kwa kushirikiana na Fiston Mayele ambaye alimzidi mbio mlinzi wa Polisi Tanzania kabla ya kumtengea Ambundo
Ulikuwa mchezo ambao Yanga iliuanza taratibu lakini ikaongeza kasi kwenye kipindi cha pili na kufanikiwa kufunga bao hilo
Ukiacha ushindi wa Yanga mlinzi Djuma Shabani huenda akafungiwa kukosa mechi tatu baada ya kumpiga kiwiko mchezaji wa Polisi Tanzania, Yahya Mbegu wakati mchezo ukielekea ukiongoni
Mwamuzi hakumpa kadi nyekundu kwa kuwa hakuliona tukio hilo lakini ni wazi kamati ya saa 72 inaweza kumuadhibu
Mbegu alianza kumkanyaga Djuma nae kuamua kulipiza kwa kumpiga kiwiko
Ni matukio ambayo sisi Wananchi hatuyaungi mkono na tunasisitiza wachezaji wetu wanapaswa kuhimili hasira zao kwani wanaweza kuigharimu timu wakati huu ambao Yanga inasaka ubingwa baada ya kuukosa kwa misimu minne mfululizo
Ushindi unaifanya Yanga ijichimbie kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama 10, baada ya kufikisha alama 35