Klabu ya Yanga inapenda kuutaarifu UMMA kuwa hairidhishwi na mwenendo wa baadhi ya Waamuzi katika ligi kuu ya NBC Tanzania Bara hasa katika michezo inayoihusisha Yanga na timu nyingine zinazoshiriki ligi kuu
Kumekuwa na mlolongo wa Maamuzi yenye utata ambayo kwa namna moja au mwingine yameinyima Yanga ushindi lakini kwa upande mwingine matukio kama hayo yamekuwa yakifumbiwa macho na kuzinufaisha baadhi ya timu zinazoshiriki ligi kuu
Tumeshuhudia matukio kadhaa ambayo yameibua mijadala mikubwa hapa nchini. Lengo wetu ni kutaka waamuzi wetu wajitafakari na pia mamlaka zinazosimamia mpira kutafakari juu ya mwenendo huu na kuchukua hatua za haraka kwani kama utaachwa tunaona utaleta athari kubwa siku zijazo
Klabu ya Yanga inasisitiza ushindani wa ligi kuu unaozingatia haki kwa upande wa waamuzi ili klabu zinazofanya jitihada kubwa ili kutengeneza timu zilizo bora zitendewe haki na waamuzi na isiwe kama ilivyo sasa ambapo waamuzi ndio wanaoamua matokeo ya michezo
Hali hii ya waamuzi kuamua nani atakuwa mshindi kwenye nchezo husika ikiendelea itawakatisha tamaa wadhamini mbalimbali wanaotoa rasilimali fedha na kuwafanya wajiondoe. Tukumbuke kuwa hilo likitokea ligi yetu itapoteza mvuto na kuathiri ubora wa ligi yetu ambayo imeanza kuwa kivutio kwa wachezaji mbalimbali
Imetolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano
Yanga Sc