Msimu huu Yanga imekamilisha michezo ya duru ya kwanza pasipo kupoteza mchezo wowote huku wakikusanya alama 39
Wananchi wako kileleni kwa tofauti ya alama nane dhidi ya watani zao Simba wanaoshika nafasi ya pili
Wapo wanaojipa matumaini kuwa pamoja na uongozi huo, Yanga inaweza isifanikiwe kutwaa ubingwa mbele ya Simba kutokana na historia ya matokeo ya misimu ya nyuma
Wengi wanatolea mfano msimu uliopita ambao Yanga iliongoza kwa muda mrefu lakini Simba ikatwaa ubingwa
Mpaka michezo ya duru ya kwanza inakamilika msimu uliopita, Yanga ilikuwa kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na alama 37 huku Simba ikiwa nafasi ya pili na alama 35
Tofauti imeonekana msimu huu ambapo Yanga imeongeza alama mbili zaidi ya walivyomaliza duru ya kwanza msimu uliopita wakati watani zao Simba wamepoteza alama nne kulinganisha na matokeo yao ya msimu uliopita

Kuna kitu Wananchi wamejifunza kutokana na matokeo ya msimu uliopita ndio maana msimu huu kila mchezo umewekewa mkazo wa aina yake
Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze ambaye msimu uliopita alikuwa kocha mkuu, amesema wao hawafikirii matokeo waliyopata kwenye duru ya kwanza wala nafasi waliyopo sasa kwani yote hayatakuwa na maana kama watashindwa kutimiza malengo yao
Ukiangalia wachezaji wana ari kubwa kila mmoja akifikiria kupata ushindi katika kila mchezo
Baada ya kukamilika kwa mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, kiungo Khalid Aucho alisema wanaanza upya ligi Jumapili, wanaanza hesabu katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar