Klabu ya Yanga imetangaza kuandaa matukio maalum kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC ambao utapigwa Jumamosi, March 19 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Msemaji wa Yanga Haji Manara amesema tukio la kwanza litafanyika siku ya kesho Alhamisi Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es salaam katika kumbukumbu ya Mwaka mmoja ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania awamu ya tano, Hayati Dk John Magufuli ambaye alifariki March 17 2021
Viongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla, GSM Foundation, benchi la ufundi na wachezaji kadhaa watashiriki kutoa misaada mbalimbali
Ijumaa Wananchi watakuwa na tukio la kuchangia damu Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Samia Suluhu Hassan
Watu 200 wa kwanza katika zoezi hilo watapatiwa jezi mpya za klabu ya Yanga ambapo Manara amesema hata kama sio mwana Yanga utapatiwa jezi ukiwa miongoni mwa watu hao
Zoezi hili litafanyika kote nchini ambapo Manara amewataka viongozi wa Matawi kufanikisha matukio ya uchangiaji damu katika mikoa yao
Siku ya Jumamosi maadhimisho ya mwaka mmoja wa Rais Samia, Wanayanga watafanya usafi katika maeneo mbalimbali jijini Dar es salaam kabla ya kuelekea uwanja wa Benjamin Mkapa kushuhudia mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC
Yanga imemuomba Rais Samia awe mgeni wa heshima katika mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa moja usiku
Aidha, siku hiyo kutakuwa na burudani za aina mbalimbali kabla ya mchezo ikiwa ni pamoja na mchezo wa utangulizi kati ya viongozi wa Yanga dhidi ya Wasanii