Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema wamejiandaa kikamilifu kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Nabi amesema KMC ni moja ya timu inayotoa ushindani kila inapokutana na Yanga
Hata hivyo wamejiwekea malengo ya kushinda mchezo huo ili kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi
"Tunakwenda kucheza na KMC, moja ya michezo ya dabi hapa Dar es salaam. Mchezo huu utakuwa tofauti na mchezo wa kwanza ambao tulishinda mabao 2-0. KMC imebadilika sasa wakiwa na kocha mwingine. Msimu uliopita wakati Yanga ikiwa chini ya kocha Juma Mwambusi tulitoshana nguvu kwa sare ya bao 1-1 hivyo tunafahamu hautakuwa mchezo rahisi," alisema Nabi
"Tunakabiliwa na michezo mitatu migumu ya dabi kwani baada ya KMC tutacheza na Azam Fc halafu Simba Sc hii ikiwa dabi kubwa zaidi"
Nabi amezungumzia utayari wa kikosi chake ambapo ametoa ufafanuzi wa kukesakana kwa Saido Ntibazonkiza ambaye kesho Jumamosi atafunga ndoa Burundi
"Saido alipata majeraha, anaendelea kuimarika. Sasa kwa kuwa yuko majeruhi uongozi ulimruhusu kurejea Burundi kukamilisha masuala yake. Tutamkosa mchezo dhidi ya KMC pamoja na Khalid Aucho, Jesus Moloko na Yacouba Songne"
"Aucho anaendelea kuimarika pengine atakuwa tayari kwa mchezo ujao dhidi ya Azam FC, Moloko pia anaendelea vizuri. Yacouba tutaendelea kumkosa mpaka mwezi Juni," alisema Nabi
Kocha huyo mwenye uraia pacha wa nchi za Tunisia na Ubelgiji, amesema katika mchezo wa kesho wachezaji Farid Mussa, Djuma Shaban na Chico Ushindi watarejea kikosini baada ya kupona majeraha