Moto wa Wananchi bado unaendelea kuziunguza timu pinzani baada ya leo kuichapa KMC mabao 2-0 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
KMC walianza vyema mchezo huo wakiipa Yanga wakati mgumu kwenye dakika 30 za mwanzo lakini wachezaji wa Yanga walionyesha ukomavu wao kwa kutumia nafasi muhimu kufunga bao kwenye dakika ya 38
Krosi ya Djuma Shabani iliparazwa na Denis Nkane kumtengenezea Fiston Mayele ambaye mpira wake ulimgonga Andrew Vicent Chikupe na kujaa kimiani
Yanga ilirejea ikiwa imara zaidi kwenye kipindi cha pili na iliandika bao la pili katika dakika ya 52 kupitia kwa Djuma Shabani aliyejaza kimiani mpira wa kona kutoka kwa Chico Ushindi
Wananchi wangeweza kuondoka na ushindi mnono zaidi kama wangetumia vyema nafasi walizotengeneza katika kipindi cha pili
Ni matokeo muhimu kwa Yanga ambayo yanaendelea kuwaimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 48
Sasa Yanga inaongoza ligi kwa tofauti ya alama 11 dhidi ya watani zao Simba wanaoshika nafasi ya pili



