Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema mchezo wa kirafiki dhidi ya Mafunzo Fc kilikuwa kipimo kizuri kwa wachezaji wake kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa April 06 uwanja wa Azam Complex na michezo mingine iliyobakia ligi kuu na kombe la FA
Mchezo huo uliopigwa uwanja wa Azam Complex juzi, uliishuhudia Yanga ikiondoka na ushindi wa mabao 3-2, Yanga ikifunga mabao yake kupitia kwa Mapinduzi Balama, Heritier Makambo na Fiston Mayele
Kaze amesema Yanga ilikuwa na idadi kubwa ya wachezaji waliokuwa wakirejea kutoka kwenye majeruhi huku wengine wakiwa hawapati nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza mara kwa mara
Kutumika kwao katika mchezo huo kumewapa benchi la ufundi taswira ya namna gani wanaweza kuwatumia katika michezo iliyosalia msimu huu
"Kuna majeruhi na kuna wachezaji wamefanya mazoezi wiki mbili hawajapata mechi yoyote, ndiyo sasa tumetaka wapate hiyo nafasi ya kucheza tuwaone walivyo, sasa kama ambavyo tumewaona waliokuwa majeruhi pia na niseme kwa ujumla kupitia hii mechi hilo limefanikiwa, imetusaidia sana kiufundi."
"Kuna vitu vilikuwa vizuri na vingine havikuwa vizuri, lakini ni sehemu ya mpira na nimefurahi haya yameonekana baada ya kufanikiwa kucheza hii mechi, ambayo imetupatia picha ya kwenda nayo katika mechi zilizobaki, maana baada ya hapa hatutapata tena muda wa kucheza mechi za kirafiki na sasa picha tuliyoipata kwa wachezaji itatuongoza mpaka mwisho wa msimu," alisema Kaze
Yanga inaingia kambini leo kukamilisha maandalizi ya mchezo dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa Jumatano ijayo katika uwanja wa Azam Complex