Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema mabingwa hao wa kihistoria hawajawahi kutegemea 'mbeleko' kutoka kwa timu yoyote kupata nafasi ya kushiriki michuano ya CAF
Bumbuli amesema msimu uliopita Yanga ilipata nafasi ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa kwa jasho lao na watafanya hivyo msimu huu
"Sisi hatujawahi kutegemea mbeleko ya timu yoyote. Msimu uliopita tulipata nafasi kutokana na jasho letu na msimu huu tutapata nafasi kutokana na jasho letu vilevile, ndio maana unaona tuko juu kwenye msimamo wa ligi"
"Tunawapongeza Simba kwa kufanikiwa kutinga robo fainali michuano ya Shirikisho na tunawatakia kila la kheri huko lakini mafanikio yao hayana athari yoyote kwetu"
"Hata kama wangetolewa mapema kusingekuwa na athari yoyote kwetu kwani tunachotazama sisi ni malengo yetu, tunahitaji kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu ili tuweze kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao" alisema Bumbuli
Tanzania ni miongoni mwa mataifa 12 ambayo yatapata uwakilishi wa timu nne kwenye michuano ya CAF msimu ujao
Ni kutokana na idadi ya pointi ambazo Tanzania imekusanya katika miaka mitano iliyopita, Simba ikichangia kwa asilimia kubwa baada ya kufika robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa mara mbili na kombe la Shirikisho
Yanga na Namungo Fc nazo zimechangia alama hizo kwani zilicheza hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Yanga ikicheza mara mbili msimu wa 2016/17 na 2018/19 huku Namungo ikicheza msimu wa 2020/21