Mikiki mikiki ya ligi kuu ya NBC inaendelea leo katika mzunguuko wa 19 wakati vinara wa ligi hiyo Yanga watakaposhuka dimba la Azam Complex kuwakabili waoka mikate wa Azam Fc katika mchezo utakaopigwa kuanzia saa 2:15 usiku
Ni mchezo mkubwa unaovuta hisia za mashabiki wa soka Tanzania, ukiacha dabi ya Kariakoo, Azam Fc vs Yanga ni mchezo mwingine unaotazamwa na mashabiki wa soka kwa wingi
Kwa Yanga ni mchezo ambao Wananchi wanazihitaji alama zote tatu ili kuendelea kuukaribia ubingwa wa ligi kuu msimu huu
Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze jana aliwaambia Wanahabari kuwa leo utakuwa mchezo mwingine tofauti kabisa na ule waliocheza uwanja wa Benjamin Mkapa na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0
Yanga leo itakosa huduma ya wachezaji Feisal Salum, Khalid Aucho ambao ni majeruhi, Farid Mussa ni mgonjwa wakati Yannick Bangala ana 50/50 ya kutumika katika mchezo huo
Vijana wa kocha Nasreddine Nabi walijichimbia kambini Avic Town kwa takribani wiki nzima kujiandaa na mchezo huo
Hautakuwa mchezo mwepesi lakini Wananchi wana nafasi kubwa ya kuendeleza ubabe wao kwenye ligi