Ni mwendo mdundo kwa Wananchi wakipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam Fc katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Azam Complex
Mabao ya Djuma Shabani (p) na Fiston Mayele yalitosha kuihakikishia Yanga alama tatu muhimu ambazo zinawaweka kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama 14 dhidi ya Simba inayoshika nafasi ya pili
Azam Fc waliuanza mchezo huo kwa kasi na iliwachukua dakika 10 kufunga bao la kuongoza kupitia kwa Rodgers Kola
Yanga ilihitaji dakika saba tu kurejea mchezoni wakisawazisha bao hilo kupitia mkwaju wa penati uliopigwa Djuma baada ya Saido kufanyiwa madhambi na mlinda lango wa Azam Fc katika eneo la hatari
Kipindi cha pili Yanga ilirejea na kasi kubwa ikisaka bao la ushindi lakini Azam Fc walitumia mbinu ya kupoza mchezo
Mayele akakata mzizi wa fitina kwenye dakika ya 78 akifunga bao bora kwa tik-tak akiunganisha krosi ya Djuma Shabani
Bao hilo unaweza kulifananisha na bao alilofunga kwenye mchezo dhidi ya Biashara United
Dakika 90 zikamalizika kwa Yanga kuondoka na ushindi huo muhimu ambao umezidi kuwasogeza Wananchi karibu na ubingwa



