Kuna wakati baadhi ya wachambuzi waliibua mjadala wakiwalinganisha mlinzi wa kulia wa Simba Shomari Kapombe na Djuma Shabani wa Yanga
Nafikiri wakati mwingine ni vyema kumuheshimu yule aliyekuzidi na iwe nafasi kwako kujifunza ili kuwa bora zaidi yake
Djuma ni mchezaji wa daraja la juu sana, walinzi wa pembeni wa Kitanzania akiwemo Kapombe kuna mambo wanapaswa kujifunza kwake
Yawezekana kuanza kwake msimu taratibu kuliwapa wengine sababu ya kumdharau, lakini wasichofahamu tembo hata akonde vipi hawezi kuwa kama sungura
Djuma ni mtambo wa kupika mabao kwenye kikosi cha Yanga. Katika michezo mitatu iliyopita amekuwa akihusika katika kutengeneza na kufunga mwenyewe
Mchezo uliopita dhidi ya KMC alisababisha bao la kwanza na mwenyewe akafunga la pili
Jana katika mchezo dhidi ya Azam Fc, amehusika katika mabao yote mawili
Krosi yake ilipelekea mlinda lango wa Azam Fc Ahmed Sarura kumfanyia madhambi Saido na kusababisha mkwaju wa penati ambao aliujaza kambani yeye mwenyewe
Akaweka krosi murua tena kwenye dakika ya 78 ambayo iliwekwa kimiani kwa ustadi sana na Fiston Mayele
Msimu huu katika ligi kuu, Djuma amehusika kwenye mabao sita, amefunga matatu na kutoa pasi za mabao matatu