Wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wa Yanga jana walishangilia kwelikweli baada ya kuishuhudia timu yao ikitinga nusu fainali ya michuano ya kombe la FA kwa ushindi wa mikwaju ya penati 7-6
Ni baada ya kulazimishwa matokeo ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Geita Gold katika mchezo ambao nusura mambo yaharibike dakika za mwishoni kabisa
Ilikuwa dakika ya 88 wakati Yanga ikitengeneza shambulizi Saido Ntibazonkiza akapoteza mpira katika mazingira ambayo ilionekana kama amefanyiwa madhambi lakini mwamuzi 'akapeta' na Geita Gold kunufaika kwa kuwashtukiza Yanga ambao walikuwa wamebakisha walinzi wawili nyuma, akaweka mpira kambani
Ni tukio ambalo lilipelekea kocha mkuu Nasreddine Nabi kutokewa kwa kadi nyekundu baada ya kumlalamikia mwamuzi
Lakini bao hilo halikuwatoa Yanga mchezoni ambapo kwenye dakika za nyongeza, mlinzi wa Geita Gold Amosi Kadikilo aliunawa mpira ndani ya eneo la hatari akiwa kwenye jitihada za kuokoa
Djuma Shabani akairejesha Yanga mchezoni kupitia mkwaju wa penati na kulazimisha mchezo huo kwenda kwenye matuta
Presha ikarejea tena upande wa Yanga wakati mlinda lango Djigui Diarra alipokosa mkwaju wa saba wa penati lakini ikawa ahueni kwa Wananchi baada ya Maka Edward wa Geita Gold nae kukosa
Diarra akaibeba Yanga mabegani kwenda nusu fainali baada ya kuokoa mkwaju wa Juma Mahadhi ambaye ndiye aliyetengeneza bao la Geita Gold
Haikuwa kazi rahisi kwa Yanga kuibuka na ushindi lakini mwisho wa siku Wananchi wakashinda na sasa wanawasubiri watani zao Simba kwenye mchezo wa nusu fainali kama watashinda mchezo wa robo fainali dhidi ya Pamba Fc
Furaha ya Wananchi imechagizwa zaidi na matokeo ya mapema kwenye ligi kuu Simba wakilazimishwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya Polisi Tanzania
Matokeo hayo yameifanya Yanga ikae kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama 10 wakiwa na alama 51 dhidi ya Simba yenye alama 41
April 30 ni mchezo dhidi ya Simba, Wananchi wanajua wakishinda mchezo huu itakuwa uhakika msimu huu watarejesha taji la ligi kuu katika mitaa ya Twiga na Jangwani kwa mara ya 28